Daniel Mjema, Moshi
WATEJA
zaidi ya 50 wa Benki ya Uchumi Commercial Bank Ltd (UCB) ya Dayosisi ya
Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) wanasakwa
na polisi kufuatia wizi wa karibu Sh250 milioni.
Vyanzo
vya kuaminika vilidokeza kuwa ingawa taarifa zilizofunguliwa polisi na
menejimenti ya UCB zinaonyesha kiasi kilichoibwa ni Sh224 milioni,
lakini kinaweza kufikia Sh250 milioni kadri uchunguzi unavyoendelea.
Benki
hiyo iliyoanzishwa mwaka 2005 baada ya kupatiwa leseni namba CBA 00031
na Benki kuu ya Tanzania (BoT), inamilikiwa na Watanzania wapatao
330,000 ambao ni waumini wa dayosisi hiyo.
Habari
za uhakika zilizolifikia Mwananchi zilisema wizi huo ulifanyika baada
ya kuparanganyika kwa mfumo wa kompyuta uliounganishwa na mashine za
ATM.
Taarifa
nyingine zilisema wizi huo ulitokana na baadhi ya wateja kuusoma mfumo
wa kompyuta hiyo na kugundua kuwa kuna nyakati za usiku huchanganyikiwa
na kutoa salio lisilo sahihi la wateja.
“Kilichotokea
ni kuwa kuna watu walivujisha siri kuwa nyakati za usiku sana
ukichomeka kadi kwenye hiyo ATM inatoa pesa hovyo hovyo hata kama hauna
salio la kutosha”kilidokeza chanzo chetu.
Uchunguzi
wa Mwananchi ulibaini kuwa wateja wa benki hiyo wapatao 50
walijihusisha na wizi wa fedha hizo kupitia ATM hiyo na tayari polisi
imeanzisha uchunguzi maalumu wa kuwasaka.
Habari
hizo zimedai kuwa baada ya kugundulika kwa dosari katika mfumo huo wa
kompyuta za ATM katika benki hiyo, baadhi ya wateja walianzisha kuchukua
fedha muda mfumo huo unapoharibika.
“Sio
pesa zilizoibwa mara moja hapana yaani unakuta leo anatoa 500,000 kesho
hivyo hivyo na ilikuwa ni wateja tofauti tofauti waliokuwa wamegundua
siri hiyo”alidokeza mtumishi mmoja wa UCB.
Baadhi
ya wanasheria walidai zipo changamoto nyingi katika kesi za aina hiyo
hasa katika kuthibitisha kama wakati mtuhumiwa anatoa fedha hizo katika
ATM,alikuwa amekula njama ya kutenda kosa hilo.
Meneja
mkuu wa Benki hiyo, Angela Moshi alipoulizwa alikiri kuwapo kwa tukio
hilo, lakini akasema hakuwa katika nafasi nzuri ya kulielezea kwa vile
alikuwa akielekea kanisani kwa ajili ya ibada.
"Naomba
uje kesho (leo)tutazugumza vizuri tu juu ya hilo jambo nitakupa
taarifa vizuri tu unajua leo ni siku ya ibada na sasa hivi naingia
kanisani kwa ajili ya ibada"alisisitiza Meneja mkuu huyo jana.
Kwa
upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro,Robert Boaz
alipoulizwa na gazeti hili juzi alisema“ni kweli hilo tukio lipo kwa
maana ya wateja ‘wame overdraw’ (wametoa zaidi) kutoka kwenye akaunti
zao na uchunguzi wa tukio hilo unaendelea”alisema Kamanda Boaz.
No comments:
Post a Comment