Mamlaka  ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), imeanza rasmi usajili kwa wananchi na  wageni wote wanaoishi nchini Tanzania kihalalai kwa lengo la kuwapatia  Vitambulisho vya Taifa.
  Kwa  mujibu wa Mkurugenzi Mkuu ndugu Dickson Maimu, zoezi hili litachukua  siku 30, na litatanguliwa na kuandikisha wakazi wote waishio  Dar-es-salaam katika daftari la makazi linalomilikiwa na serikali ya  kila mtaa. 
  Aidha  usajili wa daftari la wakazi utasajili wakazi katika kila kaya, na  maafisa usajili kwa kushirikiana na watendaji katika kila kitongozi au  mtaa watapita nyumba kwa nyumba kufanya usajili huo kabla ya kuanza  rasmi kwa zoezi la ujazaji wa fomu za usajili kwa lengo la kutoa  Vitambulisho
  Amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa maafisa na watendaji watakaohusika  na zoezi hili na kujitokeza kwa wingi katika usajili ili  katika muda uliopangwa zoezi hili kukamilika na kutoa fursa ya usajili kuendelea katika mikoa mingine ya Tanzania ili  kufikia malengo ya serikali zoezi hili kuwa limekamilika katika kipindi cha miaka miwili nchi nzima.
  Shughuli  hii imeanza rasmi tarehe 22/06/2012 hadi tarehe 21/07/2012 (kwa siku 30  tu). Walengwa katika zoezi la usajili ni watu wote wenye umri wa miaka  18 na kuendelea.
  Akifafanunua  kuhusu mahitaji ya kuwa na vielelezo, Mkurugenzi huyo amesema ni muhimu  kwa wananchi kujiandaa kuwa na vielelezo vitakavyo watambulisha ikiwa  ni pamoja na cheti cha kuzaliwa, cheti cha ubatizo, cheti cha falaki au  kadi ya kliniki vitakavyothibitisha tarehe ya mtu kuzaliwa, viengine ni  kimoja wapo kati ya cheti cha elimu ya msingi, sekondari au chuo, pasi  ya kusafiria, kadi ya mpiga kura, kitambulisho cha bima ya afya, kadi ya  mfuko wa hifadhi ya jamii, au leseni ya udereva. Amesema lengo ni  kuwezesha Mamlaka kutambua wahisika ili kutoa kitambulisho kwa raia  halali wa Tanzania, na kwa upande wa wageni ni nakala ya pasi ya  kusafiria, na kibali cha kuishi nchini (resident permit). Kuwa na  viambatanisho kutasaidia mtu kutambulika kwa haraka na kuchukua muda  mfupi kuwa amepata kitambulisho chake.
  Amesisitiza  zoezi hili ni bure halitakuwa na tozo yeyote, na fomu za usajili  zitatolewa bure katika vituo vya uandikishaji vitakavyofunguliwa katika  kila kitongoji/ mtaa.
  Mwombaji  anaweza kupata maelezo zaidi katika Ofisi Kata na Ofisi za Mamlaka ya  Vitambulisho vya Taifa zilizopo Barabara ya Kilimani, Kinondoni jirani  na Ubalozi wa Ufaransa. 
  Imetolewa na Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano (IEC)-NIDA
  23/06/2012
No comments:
Post a Comment