Na Joachim Mushi, Thehabari.com
SERA ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya Mwaka 2000, imenukuu sehemu
ya Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 na marekebisho yake ya mwaka 1984.
Sehemu hiyo inaeleza kwamba Tanzania ni nchi inayothamini usawa na haki
za binadamu. Katiba pia inasisitiza usawa na heshima kwa binadamu wote,
heshima ya kutambua na kuthamini utu wa mtu pamoja na kuhakikisha haki
mbele ya sheria.
Hata
hivyo wakati Katiba ya nchi na Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia
inasisitiza hayo bado hali ya unyanyasaji wanawake kwa vipigo nchini
Tanzania inajitokeza kwa kiasi kikubwa hasa maeneo ya vijijini. Kwa
mujibu wa utafiti wa kihabari (journalistic survey) uliofanywa mwezi
Aprili 2012 na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) kwa
kushirikiana na vyombo mbalimbali vya habari katika mikoa 20, ikiwepo 15
ya Tanzania Bara na mitano ya Zanzibar kuhusu hali ya vitendo vya
ukatili nchini. Bado suala la vipigo kwa wanawake limejitokeza kiasi
kikubwa.
Ripoti
ya utafiti huo inaonesha kuwepo kwa vipigo kwa wanawake karibu kila
wilaya iliofanyiwa utafiti. Kimsingi hili laweza kuwa tatizo kubwa la
kitaifa. Katika familia nyingi, wanawake bado wanaendelea kupigwa na
wanaume, hasa waume zao au wapenzi wao.
Na
kama hiyo haitoshi taarifa za utafiti zinabainisha kuwa yapo maeneo
ambayo hata viongozi wa kiserikali ngazi za jamii vijijini wamekuwa
wakitoa adhabu za vipigo ambazo huwaathiri zaidi wanawake. Kipigo
chochote kwa mwanamke ni kibaya kwa kuwa kinamuathiri hata katika
utendaji wake wa majukumu ya uzalishaji mali.
Takwimu
zilizotolewa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto mwaka
2000, kupitia mwongozo wa sera ya wizara hiyo zinaeleza kuwa wanawake ni
wazalishaji wakubwa hasa maeneo ya vijijini. Inakadiriwa kuwa asilimia
60 ya chakula huzalishwa na akinamama. Licha ya kundi hilo muhimu kwa
uzalishaji kuwa hodari wa kuzalisha lakini halina uamuzi juu ya mali
ambayo linaizalisha kutokana na mazingira ya mfumo na vitendo vya
unyanyasaji vikiwemo vitendo vya vipigo dhidi yao.
Lakini
utafiti wa kihabari katika taarifa yake unafafanua kwamba miongoni mwa
sababu za wanawake kupigwa ni ulevi, “mdomo” wa akina mama, ubabe wa
akinababa, fumanizi, mfumo dume, ukiukwaji wa mafunzo ya ndoa, wivu,
umaskini, “mapenzi,” ndoa za mitala, ndoa za kulazimishwa na mambo
mengine.
Pamoja na hayo sheria imeweka wazi dhidi ya adhabu kwa kipigo, Sheria ya Makosa ya Jinai Sura ya 16 ya mwaka 2002 kifungu
240 cha kinasema kwamba mtu yeyote aliyempiga mwenzake atakuwa ametenda
kosa la jinai na atahukumiwa kwenda jela kwa muda wa mwaka mmoja.
Adhabu hii itatumika katika mzingira ambayo muathirika wa kipigo hakupata madhara makubwa sana. Aidha
kifungu 241 cha Sheria ya Makosa ya Jinai kinatoa adhabu ya kifungo cha
miaka mitano jela kwa mtu yeyote aliyemdhuru mwenzake kwa kipigo na mtu
huyo kupata madhara makubwa sana.
Mfano utafiti unabainisha kuwa Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam, kwa mwaka 2011 pekee kesi 14 ziliripotiwa. Hakimu
Mkuu wa Mahakama ya Mwanzo Mbagala (PPCM) Fatuma Katunzi, anasema kesi
za vipigo zipo na kwamba mwaka 2011 zilifikishwa kesi 6, kati ya kesi
hizo 2 zilitolewa hukumu ya kifungo na faini.
Mwenyekiti
wa Mtaa wa Msufini Kata ya Chamazi, Muharami Mlawa, anasema kesi 5
ziliripotiwa katika mtaa huo. Naye Mwenyekiti wa mtaa wa Majimatitu ‘B’
Kata ya Charambe Fadhil Mpinga anasema kesi 3 za vipigo zilifikishwa
kwake. Ofisa Mtendaji Mtaa wa Mianzini Jimmy Berege, anasema uongozi wa
mtaa huo ulipokea kesi 6 kati ya kesi hizo tatu ziko polisi.
Neema
Lalashe (46) ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Uhuru Kata ya Orukasment,
wilayani Simanajiro, anasema kwa sasa vitendo vya kipigo dhidi yao
vinafanyika kistaarabu tofauti na miaka ya nyuma.
“Zamani
mwanaume alikuwa anafunga mikono na miguu kwenye mti ndiyo unachapwa,
unapigwa mpaka unapoteza fahamu lakini siku hizi kidogo hayo mambo
yamepungua, kama umekosea atakuchapa lakini hufungwi tena na kamba,”
anasema Lalashe.
Mwanamama
huyu anaamua kuhalalisha kipigo kutokana na mazoea, na anafikia hata
kuona kipigo cha nyuma kilikuwa cha kudhalilisha zaidi kuliko
kinachotolewa kwa sasa. Hali hii inaonesha ni namna gani maeneo mengine
vipigo vinazoeleka na hata kuhalalishwa kijamii kutokana na kukata tamaa
kimsaada.
Bi.
Wandoa Edward (37) mkazi wa Kijiji cha Kisiriri, Kata ya Kisiriri,
Iramba mkoani Singida, anatamani kujitoa kwenye ndoa kutokana kero za
kinyanyasaji anazozipata kwa mwenza wake. “Nataka kurudu nyumbani, kwani nimechoka kuishi katika ndoa yenye manyanyaso. Nyumba yangu si salama tena,” anasema Bi. Edward.
Mtendaji
wa Kata ya Karatu, Paulo Lagwen anakiri kuwepo kwa vipigo kwa wanawake
kutoka kwa waume zao. Anaendelea kubainisha kuwa idadi ya vipigo kwa
sasa imepungua ikilinganishwa na ilivyokuwa hapo nyuma.
Anasema
kwa Wilayani Karatu, vipigo dhidi ya wanawake vipo, ingawa ni nadra kwa
matukio haya kukuta yanaripotiwa katika vyombo vya dola. Wanaume wa
Kiiraq wamestaarabika kidogo kwa utoaji vipigo kwa sasa. Idadi ya vipigo
imepungua ikilinganishwa na hapo awali.
Mkoani
Mbeya maeneo ya vijijini, zipo ndoa nyingi zizovunjika kutokana na
kipigo kwa wanawake. Mfano kati ya watu wote 22 waliohojiwa walikiri
wanaume kuwepo wanaotoa vipigo kwa wanawake. Lucia Gwamaka mkazi wa
Kijiji cha Mpandapanda, anasema kupigwa kwa mwanamke ni jambo la
kawaida.
Kama
hiyo haitoshi tatizo la vipigo linajitokeza tena wilayani Kilolo mkoani
Iringa. Taarifa ya utafiti inabainisha kuwa viongozi wanapofikishwa
kwenye ofisi za kijiji kwa shitaka lolote viongozi hujichukulia sheria
mkononi na kuwapiga watuhumiwa.
Kwa mfano utafiti ulishuhudia
wanawake wawili ambao walikuwa na ujauzito katika Kijiji cha Kidabaga
kwa nyakati tofauti wakipigwa na viongozi wa kijiji hicho na hatimaye
mimba walizokuwa wamebeba zikaharibika kutokana na madhara ya vipigo.
Kwa mujibu wa taarifa ya utafiti inadaiwa kuwa viongozi waliohusika na vipigo hivyo ni Mwenyekiti wa kijiji cha Kidabaga,
Nicolous Katandasi na Mtendaji wa kijiji hicho, Vincent Gaifalo.
Taarifa inafafanua kuwa Mwenyekiti wa Kijiji, Nicolous Katandasi mnamo
mwezi Mei 2011 alimchalaza viboko 16 mama Silivia Kimata, kitendo
kilichosababisha mimba ya miezi mine kuharibika.
Aidha
Mtendaji wa kijiji hicho, Vincent Gaifalo alimchalaza viboko 30 Seidina
Kidwangise aliyefika kijijini hapo kumzika ndugu yake na kusababisha
mimba yake kutoka na mama huyo kupata ulemavu wa kushindwa kusimama na kutembea.
Mganga
Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Iringa, dakta Deogratias Manyama
anathibitisha kwamba hospitali hiyo Aprili 19, 2012 ilimpokea na kumlaza
Bi. Kidwangise akiwa hawezi kusimama wala kutembea na uchunguzi
ulibaini alikuwa amepoteza ujauzito huku mwili wake ukiwa na majeraha.
Jambo
la kushangaza wanakijiji hao walisema kuwa ingawa mtendaji wa kijiji
aliyempiga mama huyo na kumsababishia madhara hayo makubwa alikuwa amefikishwa polisi, hawaamini kuwa haki itatendeka dhidi yake kutokana na kushamiri kwa rushwa hapo kijijini na kwenye vyombo vya sheria wilayani.
“Ingawa
wanakijiji wa Kidabaga wamechukua hatua na kuhakikisha kuwa viongozi
hao wameondoka madarakani lakini hawajafikishwa mahakamani kujibu
mashtaka ya kuumiza wanawake na kuharibu ujauzito wao,” anasema
mwanakijiji mmoja ambaye hakutaka jina lake kiusalama.
Akina
mama wa Kimasai nao wanapigwa lakini mila zao haziruhusu kushitaki.
“Hata kama ameumizwa hawezi kusema badala yake huchinjiwa kondoo na
kupewa mafuta kama tiba,” anasema Lea Saitobiki, Mjumbe wa Halmashauri
ya Kijiji akihojiwa katika utafiti huo.
Anasema
hata kama utasikia amepigwa ukienda kumuuliza anakataa kata kata kuwa
amepigwa. Kufuatia masuala hayo kufanywa siri, hakuna takwimu
zinazoonyesha tatizo la vipigo kwa wanawake lina ukubwa gani katika kata
hiyo.
“Sisi
kama serikali tunashindwa kuingilia mambo ya kifamilia, huwezi kwenda
kwenye nyumba ya mtu ukaanza kuuliza wewe kwa nini unampiga mke wako
wakati mke mwenyewe hajawahi kuja kuripoti,” anasema Ofisa Mtendaji Kata
ya Mwembe, Athumani Mkumbwa.
Kuna
haja sasa ya Serikali kwa kushirikiana na wadau anuai kuhakikisha
inapiga vita vitendo hivi vya vipigo kwa kundi hili ikiwa ni pamoja na
kutoa elimu kwa jamii nzima, ili kuona kwamba vipigo kwa wazalishaji
mali hawa haviendelei. Hali hii itaongeza kwa kiasi kikubwa uwajibikaji
kwa kundi hili katika ngazi ya familia hivyo kujikuta inachochea
maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
*Makala haya yameandaliwa na mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com) kwa msaada wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA)
No comments:
Post a Comment