Ni kawaida ya
binadamu yeyote mwenye akili timamu anapokumbwa na tatizo kubwa kulibeba katika
uzito wake na hivyo kusitisha mipango mingine iliyokuwa kwenye ‘chaneli’.
MFANO HAI
Mfano, wazazi mejiandaa
kwenda kwenye harusi ambako mnajua mtakula na kunywa na kufurahi sana, lakini
ghafla mkiwa huko mnapigiwa simu na binti yenu na kuwaambia kuwa mti umeangukia
waya za umeme hivyo nyumbani hakuna umeme.
Mara nyingi
katika mazingira haya, wazazi hao lazima wakose raha na kuiona harusi kwao ni
chanzo cha matatizo. Hata kule kufurahi na kuserebuka kwa sana hukatika ghafla.
NI KWANINI
HUTOKEA?
Kwa kawaida
kitu kinachosababisha hali hiyo kutokea ni akili kubeba tatizo na kulilimbikiza
kichwani. Mara baada ya kuambiwa mti umeangukia waya za umeme na nyumbani ni
giza, sauti itakayokuja kichwani ni hii:
“Sasa
itakuwaje giza usiku nyumbani? Da! Ina maana ne joto hili mtalala kweli leo? Halafu
wewe umezoea kusikiliza redio usiku si utapata tabu sana, utakuwa hujui nini
kianendelea.”
“Huu umeme
umekatika leo Jumamosi ina maana mpaka Jumatatu, maana Tanesco si hawafanyi
kazi Jumapili? Lo! Hapo inamaanisha Jumatatu utakwenda kazini nguo hazijapigwa
pasi na bahati mbaya sana huna nguo zinazoweza kuvaliwa bila kupigwa pasi.”
Haya mawazo
ndiyo ambayo huondoka kabisa uwepo wa furaha ndani ya moyo.
Wako wanandoa
wanashindwa kufanya tendo la ndoa kwa sababu mtoto wao anadaiwa ada shuleni. Kwa
hiyo kila akijaribu kuurejesha mwili katika tendo, kuna sauti inasema:
“Wazazi
wenzako mtaani sijui watakuelewaje, si watakuuliza ni kwanini siku hizi mwanao
haendi shule? Utawajibu anadaiwa ada? Aibu sana, halafu wewe ulivyo smati,
unaonekana una fedha lakini kumbe ada tu inakushinda.”
Hii sauti mara
nyingi humfanya mtu ashindwe kufikiria kitu kingine. Na watu wenye kuchukuliwa
na sauti za namna hii na kuzifanyia kazi huwa wanasumbuliwa na magonjwa kama ya
moyo.
NINI CHA
KUFANYA?
Kama una mtoto
amefukuzwa shule kwa sababu ya ada, kama mzazi unastahili kabisa kufikiria
jinsi ya kutafuta fedha za ada, hilo halina ubishi. Lakini linapokuja suala la
kufanya jambo ambalo litakupa raha, lazima ulishughulikie.
Hakikisha kila
sauti inayokuja kwa lengo la kukupa hofu unaidharau na kuikejeli ukiiambia
sitaki kukusikiliza kama ni ada nitapata tu.
Aidha,
jitahidi kufikiria mambo yaliyopo kwa wakati huo kuliko kuruhusu mawazo ya
mbali. Mfano ni wanandoa, mnaweza kufikia tendo la ndoa na kujikuta mkizama
hapo mpaka mtakapomaliza ndipo mkaribishe mambo mengine.
Muda mwingi
inapokuja sauti ya hofu ipuuze kwa kutumia njia ya kukumbuka matatizo makubwa
yaliyowahi kukupata lakini yakapita kama
vile hayakuwahi kuwepo. Hii itakusaidia kuliona tatizo lililopo ni dogo sana
kuliko yaliyopita na hivyo kukufanya uweze kuweka tatizo pembeni na kula raha
kwanza.
By mwamfupe ndauka
No comments:
Post a Comment