PICHA ZA UKWELI

SIRI MPYA ZAFICHUKA

Dk. Willibroad Slaa na mchumba wake, Josephine Mshumbushi.
Josephine na Mahimbo siku ya ndoa yao.
Hati ya talaka kati ya  Josephine Mshumbushi na Aminieli Mahimbo.
Na Makongoro Oging’
SAKATA la ndoa ya Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibroad Slaa na mchumba wake, Josephine Mshumbushi limefichua siri mpya kuhusu maisha yao ya kimapenzi.
Siri hiyo, inahusu historia ya mateso aliyowahi kuyapata Dk. Slaa kutoka kwa mwanamke ambaye jina lake linahifadhiwa, kabla ya kuamua kuinua mikono na kudondokea kwa Josephine.
Imebainika kuwa wakati Slaa analo lake la kuteswa na mwanamke wake, Josephine naye ana siri inayomuumiza kutokana na yale aliyotendewa na mwanaume wake (jina tunalo), aliyekuwa naye kabla ya kutua kwa mwanasiasa huyo.
Josephine, amekiri wazi kwamba mwanaume wake aliyepita, alimtesa na kumdhalilisha kiasi cha kumfanya kuchangia mapenzi na wasaidizi wa kazi za nyumbani (ma-house girl).
Dk. Slaa, alipozungumza na mwandishi wetu mwishoni mwa wiki iliyopita nyumbani kwake, Tegeta, Dar es Salaam, alikiri kuteswa na mwanamke aliyewahi kuwa naye kabla ya Josephine kisha akaelekeza kila kitu kuhusu maisha yao na uhusiano wao, kizungumzwe na mchumba wake huyo.
Akieleza mambo kwa mtindo wa kuchambua, Josephine alisema, haoni sababu ya kutoolewa na Dk. Slaa, kwani anampenda kupita kiasi na kwamba kiongozi huyo alikutatanaye Dodoma akiwa amekondeana kwa mawazo kutokana na mateso ya mwanamke huyo (jina bado tunalihifadhi).
“Mimi na Dk. Slaa tulikutana bungeni. Mimi nilikuwa pale kama mtumishi wa bunge, yeye alikuwa pale kama mbunge wa Jimbo la Karatu. Uhusiano wetu ulianza kule. Sasa nimemtunza na amenenepeana watu wanaanza kumtamani. Huyu ni wangu.
“Watu wamuone Dk. Slaa hivi sasa, hapo kabla alikuwa anateseka. Hakuwa na mwili huu ambao watu wanamuona nao. Mwanamke wake wa zamani alikuwa anamnyanyasa, kila siku baba wa watu anashinda na kukesha kwa mawazo, sasa hivi katulia. Nampa huduma nzuri, nampikia mapochopocho ndiyo maana ananawiri,” alisema Josephine.
Aliendelea kusema, kama kuna watu wanaamini yeye hatafunga ndoa na Dk. Slaa, wanajidanganya, kwani wanazo haki za kimsingi za kutimiza azma yao.
“Mimi najua Slaa ana watoto aliozaa na mwanamke mwingine, hata mimi nimeishi na Slaa miaka minne na tumezaa mtoto mmoja. Nimeishi na Slaa bila ndoa kwa muda mrefu na sasa tumeamua tufunge ndoa Julai 21, mwaka huu,” alisema Josephine.
Aliendelea kusema: “Nitafurahi sana nikishatimiza hii azma ya kuolewa na Slaa. Ni mume mzuri hasa, namuomba Mungu akamilishe malengo yetu. Unajua huko nyuma niliwahi kuteswa na mwanaume, niliishi na mwanaume asiyejua thamani ya mke.
“Huyo mwanaume alikuwa anasababisha nichangie mapenzi na ma-house girl, kwani kila house girl niliyemuajiri, alitembea naye. Sasa hivi yote hayo yamekwisha. Dk. Slaa anajiheshimu, sina tena vurugu za mwanaume wangu kutembea na house girl.”
Kuhusu matarajio ya kimaisha, Josephine alisema kuwa anaamini panapo majaliwa baada ya kufunga ndoa na Dk. Slaa, wataishi raha mustarehe kwa sababu wanaelewana vizuri.
“Raha ya maisha ya ndoa ni kuelewana, ndiyo maana nasema sioni sababu ya mimi na Dk. Slaa kutofunga ndoa. Tunapendana na kuelewana sana. Dk. Slaa akiondoka kwangu, hatapata mwanamke atakayeelewana naye kama mimi. Hata mimi siwezi kumpata mwanaume wa kuelewana naye kama ilivyo kwangu na Slaa.
“Jambo pekee ninaloweza kuwaomba Watanzania ni kutuombea tufunge ndoa yetu salama, atukinge na maradhi ili tuendelee kuishi raha mustarehe na tuendelee kutetea masilahi yao,” alisema.
Aliongeza kuwa maandalizi ya ndoa yao yamekamilika na kilichobaki kwa sasa ni siku ifike ili watawazwe rasmi kuwa mke na mume.
KILICHOPO JUU YA DAWATI
Wakati Josephine na Slaa, wakieleza mipango yao ya ndoa, kwa upande mwingine, Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Mkoa wa Manyara, Rose Kamili, amewasilisha pingamizi mahakama kuu, akidai kuwa, Dk. Slaa ni mume wake halali.
Rose ambaye ni mzazi mwenza wa Dk. Slaa, aliwasilisha hati ya pingamizi Mahakama Kuu, akitaka pia alipwe fidia ya shilingi milioni 550.
Alitaka Dk. Slaa amlipe shilingi milioni 50 kwa kitendo chake cha kumtelekeza na watoto, akaomba pia Josephine amlipe shilingi milioni 500 kwa kitendo cha kumsababishia maumivu makali baada ya kumchukulia mume wake.
Mbunge huyo alidai kuwa yeye na Dk. Slaa walifunga ndoa ya kimila tangu miaka ya 1980, baada ya katibu huyo wa Chadema kuachana na ukasisi wa Kanisa Katoliki (Upadri), hivyo yeye ni mke halali mwenye stahili zote.
UNAKUMBUKA SAKATA LA MAHIMBO?
Awali, ilionekana kwamba pingamizi la ndoa ya Dk. Slaa na Josephine lingetoka kwa mwanaume anayeitwa Aminieli Mahimbo.
Mahimbo, alikuwa mume wa ndoa wa Josephine na ndoa yao ilifungwa mwaka 2002.
Hata hivyo, Uwazi limenasa talaka inayowatenganisha rasmi Josephine na Mahimbo, iliyotolewa na Mahakama ya Mwanzo, Manzese, Dar es Salaam, Aprili 16, mwaka huu, hivyo kuthibitisha kwamba hakuna kizuizi tena upande huo.

No comments: