Baada ya Mufti wa Tanzania Issa bin Shaaban Simba kuteua Kadhi Mkuu wa Tanzania Bara, makadhi wa mikoa 14 nao wamejulikana.
Hatua hiyo inaonesha dhahiri kuanza rasmi kwa Mahakama ya Kadhi nchini na kutaka makadhi hao kuteua siku moja kwa wiki kusikiliza kesi zitakazoletwa mbele yao. Alisema hayo juzi alipofunga semina elekezi ya siku mbili ya mashehe wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA).
Mbali na Shehe Abdallah Mnyasi kuwa Kadhi Mkuu wa Tanzania Bara akisaidiwa na naibu makadhi wakuu wawili; Shehe Abubakari Zuberi na Shehe Ally Mkoyogore, makadhi wa mikoa wamejulikana na mikoa yao kwenye mabano kuwa ni:
Shehe Masoud Jongo (Dar es Salaam)
Shehe Mustafa Shaaban (Dodoma)
Shehe Zukheir Bakhur (Tanga)
Shehe Khamis Mtupa (Pwani)
Shehe Shaaban bin Juma (Arusha)
Shehe Shaban Rashidi (Kilimanjaro)
Shehe Salum Fereji (Mwanza)
Shehe Ismail Makusanya (Shinyanga)
Shehe Abdallah Ally (Mtwara)
Shehe Shaban Salum (Tabora)
Shehe Mohamed Mshangani (Lindi)
Shehe Idrissa Kitumba (Kigoma)
Shehe Rashidi Akilimali (Rukwa)
Majaji hao waliapishwa na Mufti na kuahidi kutekeleza wajibu waliopewa kwa mujibu wa Kurani na Sunna.
Hata hivyo, ni makadhi wawili wa mikoa ya Pwani na Kigoma hawakuhudhuria ambapo Mufti aliwataka kufika Dar es Salaam na kukutana naye kwa ajili hiyo. Mufti Simba alisema makadhi wa mikoa mingine uteuzi wao utafanyika wakati wowote. Aliwataka kuwa wabunifu kwa kuratibu vizuri namna watakavyoendesha mahakama za Kadhi.
Alisema uteuzi huo unaweza kuchukuliwa kinyume na wapinzani wao, lakini lengo ni jambo hilo litulie katika taratibu zake. “Wapinzani wetu wanaweza kusema makadhi wa Bakwata, cha muhimu ni kila mmoja atimize wajibu wake bila kujali watu wengine wanasema nini na kila mtu anatakiwa apigane kwenye mkoa wake,” alisema.
Aliwataka makadhi hao wasiwe mabubu wanaposhambuliwa kwa maneno na kubughudhiwa na wasisubiri Mufti kuwatetea.
Alisema Tume ya Dini imefanya kazi yake na katika kikao hicho ilipitisha Azimio la Mufti kuwa na uwezo wa kuteua Kadhi Mkuu moja kwa moja na suala hilo litaingizwa kwenye Katiba ya nchi.
Shehe wa Wilaya na Baraza la Mashehe wanaweza kuwawajibisha Mwenyekiti au Katibu iwapo watathibitisha wanakwenda kinyume na kupeleka taarifa kwa Shehe wa Mkoa,” alisema.
“Kila mmoja anatakiwa kuwa makini anapofanya hivyo kwani anaweza kuulizwa alifanya nini na kujieleza, nilipata kushitakiwa na kudaiwa Sh milioni 500, ningezipata wapi? Lakini nikapiga dua mpaka kesi ile ikayeyuka,” alisema.
Alisema mtu anapokosea anatakiwa kuanza na onyo na kumwonya hata kumkaripia na kumwuliza kwa nini asiachishwe kazi na baada ya hapo iandikwe ripoti kwenda ngazi za juu.
“Lakini ikiwa unafanya kwa ajili ya jazba tu, inaleta misukosuko Bakwata kwani kuna wakati tuliingia migogoro ya madeni na mawakili kutokana na watu wengi kutushitaki kwa madai kuwa tumewafukuza kwa kukiuka taratibu,” alisema.
Katika azimio la pili, Tume ya Dini iliridhia tamko la Mufti la kutaka Waislamu kujitokeza kuhesabiwa, kwani ni wajibu wa Waislamu kushiriki sensa na kuacha kufanya hivyo ni kumwasi Mungu na mitume wake, kwani Waislamu wanatakiwa kuwa watii kwa Serikali yao.
Azimio lingine ni kutaka kila wilaya na mkoa kuwasilisha taarifa za utendaji kila mwezi na wajumbe wa Tume ya Dini walikubaliana kutoa semina na wahusika watajulishwa.
No comments:
Post a Comment