PICHA ZA UKWELI

Hospitali ya Rufaa Mbeya yaomba madaktari

UONGOZI wa Hospitali ya Rufaa Mbeya, imeomba serikali kuwapatia haraka iwezekanavyo madaktari wengine kuja kuziba nafasi zilizoachwa na madaktari 72 waliotimuliwa hivi karibuni.

Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk. Eliuter Samky alitoa ombi hilo kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro aliyefika hospitalini hapo kuangalia hali ya utoaji huduma kwa wagonjwa.
Dk. Samky alisema kuondoka kwa madaktari hao kumesababisha huduma katika kitengo cha upasuaji kubakiwa na madaktari bingwa wanne akiwemo na yeye wakati kitengo cha macho hakina daktari kabisa.
“Kwa kweli hali ya utoaji huduma imekuwa ngumu sana kwani tuna madaktari 39 tu hospitali nzima na Hospitali ya Wazazi ya Meta ina madaktari wawili tu waliobaki. Kwa kweli tunahitaji nguvu ya madaktari wengine kuja kutusaidia,” alisema Dk. Samky.
Akijibu maombi hayo Kandoro alisema kuwa wanafanya utararibu wa kupata madaktari wa upasuaji kutoka katika hospitali za wilaya za Kyela, Mbozi na Rungwe ili kuwapeleka Rufaa kusaidia kukidhi mahitaji ya wagonjwa.
Pia aliwaomba wakazi wa Mkoa wa Mbeya kufuata utaratibu wa kitabibu wa rufani ili kupungunza msongamano mkubwa unaoweza kujitokeza katika hospitali za Rufaa na Mkoa kwa kutibiwa katika Vituo vya Afya badala ya kukimbilia hospitali kubwa.
“Napenda kuwahakikishia wananchi kuwa licha ya kuwepo kwa upungufu wa madaktari serikali inaendelea kufanya utaratibu kuhakikisha huduma hii inarejea kama ilivyokuwa hapo awali,” alisema.
Aidha, alitumia nafasi hiyo kuwasihi wakazi wa Mbeya hususan akina mama wajawazito ambao wanahitaji huduma ya kujifungua kwa njia ya kawaida kuvitumia vituo vya afya vya Luanda, Igawilo, Iyunga na Kiwanjampaka vilivyoko katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya ili kutoa mwanya kwa wenzao wenye kuhitaji uangalizi maalum kuhudumiwa ipasavyo.
“Lakini nitoe wito kwa wakazi wa Mbeya kuvitumia vituo vyetu vya afya kwa wagonjwa ambao hawana matatizo makubwa ili kupunguza msongamano katika hospitali hii na hivyo kuwapa nafasi ya kutibiwa kwa haraka wenzetu wenye matatizo hasa wale wa dharura kama ajali,” alisisitiza Kandoro.
Mkuu huyo wa mkoa pia alitembelea hospitali za Ifisi ambayo ni Hospitali teule ya Wilaya ya Mbeya pamoja na hospitali ya Mkoa ambapo alijionea hali ya mlundikano wa wagonjwa hususan wale wa nje (OPD) na kuelezwa changamoto kadhaa zilizojitokeza hospitalini hapo kutokana na mgomo wa madaktri.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk. Seif Mhina, alimweleza mkuu wa mkoa kuwa baada ya huduma kusuasua katika Hospitali ya Rufaa pamoja na ile ya wazazi Meta, kina mama wanaohitaji kujifungua wamekuwa wakielekea hospitali ya mkoa, jambo ambalo limeifanya kuelemewa na wagonjwa.
“Sasa changamoto kubwa inakuwa ni katika vifaa tiba pamoja na dawa kwa kuwa tunapokea wagonjwa wengi sana hivi sasa kulinganisha na uwezo wetu, lakini pia tungeomba kuongezewa manesi ambao watasaidia upande wa kina mama kujifungua,” alisema.
By
Habari Dullonet

No comments: