PICHA ZA UKWELI

Meja Jenerali Kisamba:Tanzania na Watanzania Amkeni na Mchangamkie Fursa za Uwekezaji na Biashara Ambazo Zimejitokeza Nchini Sudani ya Kusini

  Meja Jenerali Wynjones Kisamba, Naibu Kamanda wa Vikosi vya kulinda amani katika Jimbo la Darfur akibadilishana mawazo na baadhi ya maafisa wa Ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, katika mazungumzo yake na maafisa hao, Meja Jeneral amezungumza kwa kina fursa za uwekezaji zilizopo katika nchi ya Sudani ya Kusini namna gani Tanzania na watanzania kama wakijipanga na wakithubutu watakavyoweza kunufaika na fursa hizo ambazo amesema kwa sasa zimechangamkiwa sana na majirani zetu ili hali Tanzania bado tukisuasua. Akazungumzia pia kuhusu operesheni ya kulinda amani huko darfur na changamoto zake, lakini pia uwepo wa fursa ya Tanzania kupanua ushiriki wake katika eneo hilo.
Baadhi ya Maafisa wa Ubalozi wakiwa katika picha ya pamoja na Meja Jenerali Kisamba, ambapopia alitumia mazungumzo yake na maafisa hao kuwashukuru na kwa kazi nzuri ya kuiwakilisha Tanzania katika Umoja wa Mataifa, huku akiwataka kuto legeza kamba katika kutetea maslahi ya nchi na vile vile kutoa ushauri endelevu katika masuala mbaliambali yanayohusika na utekelezaji wa majukumu yao. 
--
Na Mwandishi Maalum

Ushauri umetolewa kwa Tanzania na Watanzania kuamka na kuchangamkia fursa za uwekezaji na biashara ambazo zimejitokeza nchini Sudani ya Kusini.

Ushauri huo umetolewa siku ya Jumatano na Meja Jenerali Wynjones Kisamba, Naibu Kamanda wa vikosi vya kulinda amani katika jimbo la Darfur maarufu kama UNAMID, wakati alipokutana na kubadilishana mawazo na maafisa wa Ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, New York.

Meja Jenerali Kisamba yuko hapa Umoja wa Mataifa, kwa ziara ya kikazi na mafunzo ya maafisa wa ngazi za juu katika misheni za Umoja wa Mataifa, mafunzo ambayo yameandaliwa na Idara ya Operesheni za Ulinzi wa Amani ya Umoja wa Mataifa (DPKO).

“ Tanzania tuna kila sababu ya kuwekeza nchini Sudani ya Kusini, zipo fursa nyingi mno kuanzia upelekaji wa chakula hadi ujenzi. Nilikuwa nyumbani hivi karibuni, nimekutana na viongozi mbalimbali na kuwaelezea juu ya fursa hizi”. Akasema Meja Jenerali

Na kuongeza.” Lakini wasiwasi wangu ni kwamba tunachelewa wakati majirani zetu wamekwisha zichangamkia fursa hizo na wako mbali sana sasa, kwa maneno mengine naweza kusema wameishaingia mpaka jikoni” alisema Meja Jenerali huyo kwa hisia kubwa.

Aidha katika mazungumzo yake na maafisa wa ubalozi, Naibu Kamanda wa vikozi vya UNAMID amebainisha kwamba kama kweli serikali, kwa kushirikiana na sekta za umma na binafsi zikiamua kuingia kibiashara Sudani ya Kusini hakuna tutakachopoteza.

“Sudani ya Kusini ndio kwanza wanaanza kuijenga nchi yao, wanachangamoto nyingi, sisi tunaweza kuwasaidia kwa maana ya kuwekeza na kwa kufanya biashara. Kwa mfano wale wanakula sana chapati, hawana ngano, tunaweza kuwauzia ngano, wanahitaji mafuta ya kupikia tunayo alizeti, wanahitaji vifaa vya ujenzi, tuna viwanda vya saruji na nondo pia, kwa kweli fursa zipo tunachotakiwa ni kujipanga tu na kuwahamasisha wafanyabiashara wetu. Lakini kubwa na la msingi zaidi, lazima Watanzania tukubali kuthubutu”. Amesisitiza Meja Jenerali Kisamba.

Akielezea kuhusu suala zima la operesheni za kulinda amani huko Darfur, eneo ambalo yeye ni Naibu Kamanda akiongoza bataliani 17 zenye wanajeshi wapatao17,364 wakiwamo polisi 5,511 kutoka nchi 52, Jenerali huyo alisema kuwa, kama ilivyo katika fursa za uwekezaji, Tanzania pia bado inayo fursa kubwa ya kujiimarisha zaidi katika eneo la ulinzi wa amani.

Akaeleza kwamba, wanajeshi kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) pamoja na askari polisi wanaohudumu katika jimbo la Darfur wameonesha uhodari wa hali ya juu kiasi cha kupigiwa mfano na mataifa mengi makubwa.

“ Siyo kama najisifu, lakini watu wetu wameonesha uhodari na maarifa ya hali ya juu, wanafanya kazi nzuri, wanaheshimika, wananidhamu, wanaitangaza vema Tanzania” akasema

Na kusisitiza. “Tumekuwa tukizungumzwa vizuri sana na baadhi wa washirika wetu kama vile Norway na Sweden. Na hii inatupatia fursa ya kujipanga vizuri zaidi kwa maana ya kuwaandaa na kuongeza idadi ya wanajeshi na askari polisi katika eneo hilo”, akabainisha Jenerali Kisamba.

Kwa mfano, akasema licha ya mahitaji makubwa ya wanajeshi, lakini kuna hitajio kubwa la askari polisi na hasa wanawake.

“ Tunahitaji kuwekeza katika raslimali watu kwa maana ya wanajeshi wetu na polisi wetu. Wanajeshi wetu ni wazuri mno, na polisi wetu ni wazuri pia, lakini, na hasa kwa polisi wetu na kwa kuwa ndo wameanza karibuni. Hawa wanahitaji mafunzo zaidi katika ngazi ya kimataifa kutokana na ukweli kwamba mafunzo wanayopewa ni yale ya kukidhi mahitaji ya ndani ya nchi. Lakini ni kundi linahohitajika sana hivi sasa katika operesheni za kulinda amani”. akasema

Aidha kwa kulitambua hilo, ameeleza kwamba michakato mbalimbali inafanyika, ambayo pamoja na mambo mengine, inahusisha kuwajengea uwezo na maarifa wanajeshi na polisi ili waweze kukidhi mahitaji na viwango vya kimataifa. Jambo litakalo rahisisha uwapo na utayari raslimali watu tayari kuhudu katika operesheni za kulinda amani mara tu tunapoombwa na jumuia ya kimataifa kufanya hivyo.

Akizungumizia hali ilivyo katika jimbo hilo la Darfur na maeneo mengine kwa ujumla, Meja Jenerali Kisamba amesema kuwa, ingawa wanajeshi wa kulinda amani wanajitahidi sana kutekeleza majukumu yao, lakini kusema ule ukweli hadi sasa hakuna amani ya kulinda jimboni Darfur.

Hata hivyo, akasema wanajeshi na polisi waliopo katika eneo hilo wanaendelea kutekeleza majukumu yao, yakiwemo yale ya kulinda raia, jukumu ambalo linabaki kuwa kati ya majukumu makubwa kabisa ya UNAMID.

Kwa upande wake, Tanzania kwa sasa inacho kikosi kimoja cha kijeshi, kombania moja ya wahandisi wa medani, waangalizi wa amani na maafisa wanadhimu pamoja na polisi washauri. Ambao idadi yao yote kwa ujumla hadi kufikia mwezi Mei 2012 inafikia jumla 1,330.

Idadi hiyo inafanya nchi yetu kuwa katika nafasi ya 19 kidunia kati ya nchi 115 zitoazo walinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa duniani.

No comments: