PICHA ZA UKWELI

Lori lagonga basi la abiria Tegeta; Laua wawili papo na kujeruhi wanane

 
picha via Michuzi blog
Taarifa ya habari TBC ya saa saba imetangaza kutokea kwa ajali mchana wa leo huko Tegeta ambayo ililihusisha lori la mchanga lenye namba za usajili T 376 AZH, na basi la abiria "daladala" lenye namba za usajili T 761 AJC, katika eneo la Njia Panda ya kuelekea kwenye kiwanda cha saruji cha Wazo Hill, Tegeta, Dar es Salaam na kusababisha vifo pamoja na majeruhi.

Imeelezwa kuwa lori hilo lililokuwa limebeba kifusi likiwa katika mwendo kasi, breki zake zilifeli na ndipo lilipoigonga 'daladala' hiyo ifanyayo safari zake kati ya Kariakoo na Tegeta (kama inavyosomeka pichani), wakati huo ikiwa na abiria ikitokea Kariakoo, kabla ya kuparamia baa ya KMM & Pub inayomilikiwa na Kuwedi Mongi iliyokuwa jirani na eneo la ajali.

Ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu wawili papo hapo, mmoja wao akiwa ni mama lishe aliyetambulika kwa jina Halima Salumu (35) na mwanaume aliyekuwa amesimama kutuoni, ambaye hakuweza kutambulika mara moja.

Akiwa kwenye eneo la tukio, Kamanda wa Polisi mkoa wa kipolisi wa Kinondoni, Charles Kenyela amewataja majeruhi kuwa ni Peter Magayane, Frank Mmari, Ramadhani Rashid, Stanley Shenge, Agnes Shadrack, Jane Kimaro, Anna Sahute na Ewina (jina moja) ambao wote walikuwa abiria ndani ya daladala hiyo.

No comments: