KAMBI rasmi ya Upinzani Bungeni imetaka kuchunguzwa kwa madai ya Naibu Kiongozi wa wa kambi hiyo, Zitto Kabwe, kuhongwa. 
  Kambi hiyo pia imetaja majina ya wabunge sita wa Chama Cha Mapinduzi 
(CCM), waliokuwa wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini iliyovunjwa na 
Spika wa Bunge, Anne Makinda, mwishoni mwa wiki, ikidai kuwa kwa namna 
moja ama nyingine walihusika na vitendo vya rushwa. 
  Wabunge hao wanatuhumiwa kupokea rushwa kutoka kwa kampuni za mafuta 
ili kuipigia debe menejimenti ya Shirika la Ugavi wa umeme nchini 
(TANESCO). 
  Akizungumza jana na waandishi wa habari mjini hapa, Mnadhimu Mkuu wa 
kambi hiyo, Tundu Lissu, alisema wamesikia tuhuma nyingi dhidi ya Zitto 
lakini hawajamhoji kiongozi huyo. 
  Alisema wanaviomba vyombo vinavyohusika vimchunguze Zitto ili ukweli 
ujulikane na hatua zinazostahili zichukuliwe kama atathibitika kuwa na 
makosa. 
  “Chama hatujakaa na Zitto kumsikiliza lakini tunataka achunguzwe, hatuna masilahi yoyote katika uchafu huu wa rushwa. 
  “Uchunguzi huu utatupa msingi wa kumchukulia hatua kama chama ikiwa itathibitika amehongwa,” alisema. 
  Alibainisha kuwa, mbunge wao huyo amekuwa akihusishwa na kumtumia 
ujumbe mfupi wa vitisho Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, Eliakimu 
Maswi. 
  Alisema ni vema Zitto achunguzwe na apewe nafasi ya kujieleza kama 
itakavyokuwa kwa wengine kuliko kuendelea kusambaza maneno ya 
kufikirika. 
  Alibainisha wamejiridhisha pasipo shaka kuwa wabunge wao watatu 
waliokuwa wajumbe kwenye Kamati ya Nishati na Madini, John Mnyika 
(Ubungo), David Silinde (Mbozi Magharibi) na Mwanamrisho Taratibu Abama 
(Viti Maalumu), hawajahusika kwa lolote katika sakata hilo la rushwa. 
  “Kama kuna mtu ana ushahidi zaidi ya huu tulionao tunaomba atuletee 
ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa, lakini mpaka sasa wabunge wetu hawa 
watatu hawajashiriki kwa lolote katika kuomba rushwa,” alisema. 
  Kauli ya Lissu inashabihiana na aliyoitoa Zitto juzi ambapo alisema 
hajachukua hongo, ila kuna watu wana lengo la kuchafua jina lake. 
  Zitto alisema kuwa uchunguzi dhidi yake ndiyo njia pekee ya 
kuudhihirishia umma kuwa hahusiki na chochote kama baadhi ya watu 
wanaoeneza maneno ya kumchafua. 
Awataja wala rushwa 
Kuhusu majina ya wabunge wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya 
rushwa, Lissu alisema kuwa kwa mujibu wa kanuni za kudumu za Bunge na 
Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1995, wabunge hao 
walipaswa kutaja masilahi yao kibiashara kwenye shirika hilo. 
  “Sasa wabunge hawa hawajawahi kufanya hivyo na wameendelea kuwa 
wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini na wengine kufanya biashara na 
TANESCO,” alisema Lissu na kuwataja kuwa ni Munde Tambwe, Sara Msafiri, 
Mariam Kisangi wa Viti Maalumu, Yusuf Nassir (Korogwe Mjini) na Charles 
Mwijage Muleba Kaskazini. 
  Lissu alifafanua kuwa Tambwe na Msafiri wana tenda ya kuiuzia TANESCO 
matairi na kwamba hawajawahi kutangaza masilahi yao katika jambo hilo 
kwenye kamati zao. 
  “Mwijage ni mtaalamu mwelekezi wa Kampuni ya PUMA Energy iliyopewa 
tenda na Maswi kuiuzia mafuta TANESCO, hivyo kama mjumbe wa Kamati ya 
Nishati ana mgongano wa kimasilahi. Nassir na Kisangi hawa wanafanya 
biashara ya mafuta wanamiliki vituo vya mafuta na wana mgongano,” 
alisema. 
  Kuhusu Christopher ole Sendeka, Lissu alidai kuwa amekuwa akizipigia 
debe kampuni tatu zilizonyimwa tenda ya kuiuzia mafuta TANESCO 
akiwashawishi wajumbe wa kamati kuwa serikali ilikiuka kanuni kuipa 
tenda Kampuni ya PUMA Energy. 
  Mbunge mwingine aliyetajwa ni Vicky Kamata wa Viti Maalumu ambaye alidaiwa kuwa na mgongano wa kimasilahi na Maswi. 
  “Tunampongeza Spika kwa kuivunja Kamati ya Nishati na Madini lakini 
tunataka azivunje pia zile za LAAC, inayoongozwa na Augustine Mrema 
(TLP) na POAC ya Zitto, kwa kuwa baadhi ya wajumbe wake wamekuwa 
wakitajwa sana kujihusisha na vitendo vya rushwa. 
  Fukuto la kutajwa kwa majina ya wabunge wanaotuhumiwa kwa rushwa 
lilitawala mjadala wa Bunge jana, ambapo wabunge, Kangi Lugora 
(Mwibara), James Mbatia (Kuteuliwa), Ali Keisy (Nkasi), Joshua Nassari 
(Arumeru Mashariki na Salum Baruani (Lindi Mjini), waliomba mwongozo wa 
Spika wakidai wahusika wawekwe wazi. 
  Hata hivyo, katika mwongozo wake, Naibu Spika, Job Ndugai, alisema 
kuwa Kamati ya Maadili, Haki na Madaraka ya Bunge inaendelea na 
uchunguzi kama ilivyoagizwa na Spika ndipo hatua nyingine zitafuata. 
  “Wabunge, baadhi mtaitwa kusaidia kamati hiyo lakini si kwamba ukiitwa
 kuhojiwa na kamati inamaanisha umepokea rushwa, ni katika hatua za 
mwanzo tu kufikia ukweli wa kile kinachochunguzwa. Labda niwaeleze kuwa 
Spika amekubali kuiangalia kamati hii ili wale wajumbe wenye mgongano wa
 kimasilahi waondolewe,” alisema. 
  Alikataa kutaja majina ya watuhumiwa akisema kuwa Spika pamoja na yeye
 hawawajui wahusika ndiyo maana wanachunguza kuwabaini. Lakini aligusia 
kuwa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU), imeanza 
kuwahoji baadhi ya wabunge. 
  Ndugai pia alitolea ufafanuzi mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Tabora 
Mjini, Ismail Rage (CCM), aliyetaka kujua ni kwanini kiongozi wa 
upinzani alitaja majina ya watuhumiwa wa rushwa kutoka CCM wakati kwenye
 chama chake cha CHADEMA kuna watuhumiwa pia. 
  “Mimi ningewashauri kuwa katika jambo hili tuwe na subira na tukitaka 
kulizungumza tutende haki kwa pande zote, maana hakuna chama chenye sera
 ya kura rushwa, tusilifanye kisiasa kwa kuoneana,” alisema Ndugai. 
Watuhumiwa wajitetea 
Tanzania Daima iliwasiliana na watuhumiwa kujua wana kauli gani dhidi
 ya tuhuma hizo ambapo Mwijage, Msafiri na Munde simu zao ziliita pasipo
 kupokewa wakati Ole Sendeka, Kisangi na Nassir walizikanusha. 
  Nassir alisema kuwa si kweli kuwa anafanya biashara ya mafuta bali 
aliwahi kufanya kazi katika Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) 
ambapo alipata ujuzi na hivyo kuwa na nia ya kutaka kuanza biashara ya 
gesi. 
  “Lissu ni mwanasheria lakini nashindwa kuelewa ni kwanini anafanya 
‘generalization’ katika jambo hili, mimi sifanyi biashara ya mafuta na 
TANESCO wala serikali kupitia wizara husika, nampuuza kwa madai yake na 
nitamchukulia hatua,” alisema. 
  Kwa upande wake Kisangi alikiri kufanya biashara ya mafuta, akisema 
anamiliki vituo vya mafuta eneo la Mbagala Rangi Tatu, lakini akafafanua
 kuwa kila wakati alipochangia hoja ndani ya Bunge na kwenye Kamati ya 
Nishati na Madini alitangaza masilahi yake. 
  “Mimi niko vizuri sina wasiwasi, rejea kumbukumbu rasmi za Bunge 
utaona kuwa nimetangaza masilahi yangu, hivyo namshangaa huyu 
mwanasheria. Ina maana naye kuwa kwenye Kamati ya Sheria ni mgongano wa 
masilahi kwa vile ni mwanasheria?” alihoji. 
  Ole Sendeka naye alisema kuwa hakuwahi kuzipigia debe kampuni 
anazohusishwa nazo kwani alichokifanya kwenye kamati ni kuwaeleza 
wajumbe namna Maswi alivyovunja sheria ya manunuzi ya umma. 
  “Maswi ameichukua PUMA Energy kama mashati ya mitumba sokoni wala 
haikuwa kushindanishwa, sasa kama Lissu ambaye ni mwanasheria haoni hilo
 napata taabu,”  
 |