PICHA ZA UKWELI

WALIMU IRINGA KUANZA MGOMO LEO ?



Rais wa CWT: Gratian Mukoba
BAADA ya mgomo wa madaktari kumalizika Taifa limeendelea kuandamwa na jinamizi la migomo hiyo baada walimu kubariki kuwepo kwa tishio la mgomo wa walimu wa shule za msingi hapa nchini limeendelea kupamba moto mkoani Iringa baada ya orodha kubwa zaidi ya asilimia 90 ya walimu katika shule za Manispaa ya Iringa kubariki kuanza mgomo wao leo .
Tishio hilo la mgomo linakuja huku shule zikitarajiwa kufunguliwa siku hiyo ya jumatatu jayo Julai 9 jambo leo limebaini kuwepo kwa maandalizi makubwa ya zoezi la walimu kujiandikisha ili kushiriki mgomo siku hiyo ya kufungua shule .
Japo zoezi hilo la kujiorodhesha linaendeshwa kwa siri na walimu hao kwa ushauri kutoka chama cha walimu wilaya mkoa na Taifa katika kuunga mkono tamko na azimio la kuitisha mgomo nchi nzima lililotangazwa na Chama cha Walimu (CWT).
Katika Mkoa wa Iringa, walimu wengi wameunga mkono mgomo huo na kwamba wako tayari kugoma Jumatatu na liwalo na liwe dhidi yao.
Mgomo huo umeitishwa na CWT ikitaka Serikali iwaongeze walimu mshahara kwa asilimia 100, posho kwa walimu wa sayansi kufikia asilimia 55 ya mshahara wao, walimu wa sanaa kulipwa posho ya asilimia 50 ya mshahara, walimu wanaofanya kazi katika mazingira magumu wapewe asilimia 30 ya mshahara wa mwezi.
Mgomo huo wa walimu unakuja wakati hali ikiwa tete kufuatia mgomo wa madaktari ambao bado haujapatiwa tiba.
Katibu wa Chama cha walimu (CWT) Manispaa ya Iringa, Peter Mvilli alinukuliwa na gazeti la kila wiki linalotolewa mkoani Iringa la Kwanza jamii Iringa kuwa viwango vya mishahara vya walimu vilivyopo sasa ni vidogo, vikiongozwa kwa asilimia 100 havitakuwa mzigo kwa serikali.
A, posho zinazodaiwa na walimu ziliwahi kulipwa katika kipindi cha utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi ambapo zililipwa kila kila mwisho wa mwezi wa kulipa mshahara.
“Mheshimiwa Mwinyi aliheshimu posho za kipindi chote cha utawala wake, lakini Rais Benjamin Mkapa aliziondoa,” alisema.
Kwa mjibu wa Mwalimi Mvilli, Mkapa aliamua aziunganishe kwenye mshahara na Waraka wa Serikali ulieleza hivyo, lakini kadiri siku zilivyozidi kusonga hakuna mwalimu aliyekuta mshahara uliounganishwa na posho.
“huo ulikuwa usanii, posho hazikuingizwa kwenye mshahara mpaka leo,” alisisitiza.Alifafanua kuwa mgomo wa walimu unaotakiwa kufanyika nchi nzima, umezingatia hatua zote za kisheria na tayari kwa upande wake ameshawaelimisha walimu wa Manispaa ya Iirnga na idadi kubwa wako tayari kuungana na wenzao nchini kugoma ili kuishinikiza serikali kuwalipa madai yao.
“Tayari walimu wameshaanza kupiga kura kwa ajili ya kuunga mkono au kupinga mgomo huo unaotarajiwa kufanyika Julai 9, mwaka huu,” alieleza.
Aidha licha ya walimu wengi katika Manispaa ya Iringa kuunga mkono mgomo huo, baadhi ya walimu wamepinga hatua hiyo wakieleza kuwa wao hawawezi kuigomea Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
“Shule ya Msingi Mlangali ina walimu 20, waliounga mkono ni 18 wawili wamepinga na sababu waliyotoa ni kuwa, kuigomea CCM kwao ni dhambi,” alisema katibu huyo.
Gazeti hili linayo nakala ya taarifa ya maandalizi ya mgomo ambayo imeonyesha walimu wengi wa Manispaa ya Iirnga wakiwa wameunga mkono hatua ya mgomo. Shule za Msingi Mawelewele, Maendeleo, Kibwabwa, Viziwi, Kihesa na Shule za Sendari Lugalo na Mlandege ndizo ambazo walimu wake wote wameafiki kugoma.
Katika hatua nyingine, baadhi ya wananchi waliohojiwa na gazeti hili wiki iliyopita walisema kazi kazi ya ualimu haina maslahi kwa wahusika, kwani wengi wanaonekana kuishi maisha ya taabu.
Rosta Kajuni, mkazi wa Ipogolo, Manispaa ya Iirnga aliliambia gazeti hili kuwa, maslahi wanayopata walimu hayaendani na kazi kubwa waifanyayo.
“Hii imesababisha hata kiwango cha elimu kushuka kwa sababu walimu wamekuwa hawafundishi vizuri. Pia mazingira yao ya kazi ni mabovu, kwa mfano hapo Ipogolo, nyumba za walimu hazina umeme,” alisema. Mkazi mwingine wa Manispaa, Frank Mwangosi alisema kazi ya ualimu haiendani na maslahi yao, kwa sababu hata nyumba za kukaa hawana na wale walio nazo huwa hazina huduma muhimu kama umeme na maji.
“ Wengine wanaishi mbali na shule lakini hawana usafiri wa kuwawezesha kufika vituo vyao vya kazi. Ndio maana hata kasi yao ya ufundishaji huwa iko chini,” alieleza. Tuombe Malekano, mkazi wa Manispaa, pia alilieleza gazeti hili kuwa mishahara ambayo walimu wanalipwa haiendani na mfumuko wa bei uliopo hivi sasa.
Taarifa kutoka kwa walimu mbalimbali nchini zilieleza kwamba,Serikali inatakiwa kuwaongeza mishahara na posho ifikapo Julai Mosi, kinyume chake hawataingia madarasani kufundisha. Mbali ya nyongeza ya mishahara na posho, walimu wengi nchini bado wanaidai serikali malimbikizo ya madai yao mbalimbali, ambayo pia wataka walipwe ndani ya siku thelathini ambazo zinaishia Julai 8, mwaka huu.
Kwa sasa shule nyingi za Msingi na Sekondari nchini zitafunguliwa Julai 9, siku ambayo walimu wamepanga mgomo. Mapema mwezi Machi mwaka huu, Kaimu Katibu Mkuu wa CWT, Ezekiel Oluoch, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema walimu wataendelea kugoma na kufanya maandamano iwapo serikali itashindwa kutekeleza ahadi za kulipa madeni yao.
Hata hivyo mgomo huo wa walimu umeanza kupokelewa tofauti na wakazi wa manispaa ya Iringa huku baadhi ya wazazi wakiunga mkono uwepo wa mgomo huo na baadhi wakipinga kwa madai kuwa kufanya hivyo kutasababisha wanafunzi waliopo darasa la saba kufeli zaidi mwaka huu

No comments: