PICHA ZA UKWELI

VIJANA WATAKIWA KUJIAJIRI KUPITIA KILIMO NA UJASIRIAMALI


 


Na mwandishi wetu

 

VIJANA wametakiwa kutumia juhudi na maarifa ili kuweza kujiajiri kupitia kilimo na ujasiriamali badala ya kusubiri ajira katika taasisi za serikali pekee.

 

Pia, wametakiwa kujiunga katika vikundi ili kupata fursa za kupata mikopo katika taasisi za fedha ili kuwawezesha kuanzisha miradi ya maendeleo.

 

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Tanzania Youth Development Agency (TAYODA), Jackson Kangoye, wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam, jana, kuhusu masuala mbalimbali ya taasisi hiyo.

 

Alisema vijana nchini wamekuwa na changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa ajira licha ya kuwa na elimu na maarifa ya kutosha na kwamba, njia pekee ya kujikwamua ni kuanzisha miradi ili kuweza kujiajiri na kujipatia kipato.

“Ulimwenguni kote kwa sasa kuna tatizo la ajira na hali ya uchumi ni mbaya, lakini hili lisiwavunje nguvu vijana wenzetu na badala yake tujipange ili kuweza kujiajiri kwa kuanzisha miradi ya ujasiriamali. Tutumie vikundi ili kupata fursa za mikopo kwenye taasisi za fedha nchini, hili ndiyo litakuwa jambo la msingi kwetu,” alisema Kangoye.

 

Kuhusu mikakati ya TAYODA kuanzisha benki ya vijana, Kangoye alisema mchakato unaendelea na kwa sasa wapo katika hatua nzuri kwani, wamekuwa wakipata ushirikiano kutoka kwa watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa serikali.

 

Alisema lengo la kuanzishwa kwa benki hiyo ni kuwawezesha vijana kuondokana na kero mbalimbali ikiwemo tatizo la ajira kwani, wataitumia kukopa fedha za kuanzisha miradi.

 

“Kuna benki na taasisi nyingi za fedha nchini zinazotoa mikopo, lakini fursa hiyo kwa vijana walio wengi hawaipati kutokana na kukosa dhamana. Hii itakuwa tofauti kwa kuwa itakuwa na utaratibu maalum na makini wa kuwatambua vijana na shughuli wanazotarajia kuanzisha hivyo kuwawezesha kwa urahisi,” aliongeza Kangoye.

 

Kangoye alisema tathimini ya kina imeshafanyika na wataalamu wameridhika nayo, hivyo kwa sasa wapo katika hatua ya kufanya mchanganuo yakinifu ili kukidhi haya ya kijana wa Kitanzania.

 

"Taasisi imekuwa ikiwahamasisha vijana hasa walioko vyuoni kujikita kwenye ajira binafsi ikiwemo ya kilimo kupitia sera ya kilimo kwanza. Kwa sasa tunaendelea na utaratibu wa kuwawezesha vijana na tumeanza kutoa matrekta madogo kwa shughuli za kilimo," alisema.

 
Kwa sasa TAYODA ina zaidi ya wanachama 8500 wakiwemo wanafunzi wa elimu ya juu pamoja na matawi yake manane kutoka vyuo mbalimbali nchin

No comments: