MDHIBITI NA MKAUGUZI MKUU AKABIDHIWA RASMI UJUMBE WA BODI YA UKAGUZI YA UMOJA WA MATAIFA
Na Mwandishi Maalum
Ofisi
ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, imekabidhiwa rasmi Ujumbe wa Bodi ya Wakaguzi ya
Umoja wa Mataifa ( UNBOA)
Makabidhiano
hayo yamefanyika siku ya Jumatano hapa Makao Makuu ya Umoja wa
Mataifa, katika hafla iliyofanyika mwishoni mwa mkutano wa 66 wa Bodi ya
Wakaguzi ya UM.
Katika
hafla hiyo Afrika ya Kusini ndiyo iliyoikabidhi Tanzania kijiti hicho.
Makabidhiano ambayo yalishuhudiwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe.
Balozi Ombeni Sefue ambaye ameiwakilisha Serikali katika makabidhiano
hayo.
Afrika ya Kusini imekuwa mjumbe wa Bodi kwa miaka 12 na Tanzania itamaliza ngwe yake mwaka 2018
Aidha
hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Bi Suzan Malcora ambaye ni Msimamizi
Mkuu wa Ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (Chief de Cabinet).
Akimwakilisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe. Ban Ki Moon.
Akizungumza
wakati wa hafla hiyo iliyowashirikisha pia wajumbe wengine wa bodi
ambao ni Bw. Dong Dasheng akimwakilishi Mkaguzi Mkuu kutoka Uchina na
Bw. Amyas Morse Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu kutoka Uingereza. Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu , Bw. Ludovick Utouh amewahakikisha wajumbe wenzie
pamoja na sekretariati ya Umoja wa Mataifa kwamba Ofisi yake imejipanga
vema kulibeba jukumu hilo.
“
Hafla hii ya leo inahitimisha rasmi mchakato mrefu wa makabidhiano ya
jukumu hili, mchakato ulioanza tangu uteuzi wangu ulipofanyika mwezi
Novemba mwaka jana. Ni mchakato unaofungua ukurasa wa kubadilishana
mawazo, uzoefu na utaalamu. Kwa niaba ya Nchi yangu, Ofisi yangu na mimi
mwenyewe binafsi naomba nitoe shukrani zangu za dhati kwa wajumbe wa
Bodi ya UM na Kamati ya Operesheni za Ukaguzi” akasema Bw. Otouh.
Akabainisha
kwamba Tanzania inachukua jukumu hilo la kuwa mjumbe wa UNBOA katika
kipindi muhimu, kipindi ambacho UM unapita katika mageuzi makubwa ya
kubadili mifumo yake ya kiutendaji ikiwamo kutoka utumiaji wa mfumo
ujulikanao kama UNSAS kwenda mfumo wa IPSAS.
“
Tunaingia katika bodi hii katika kipindi ambacho UM inapitia mageuzi
makubwa yakiwamo yale ya kutoka ukaguzi uliokuwa ukifanyika kila baada
ya miaka miwili na kuingia katika ukaguzi wa kila mwaka”. Akasisitiza
Otuoh
Na
kuongeza. “ Matokeo ya mageuzi haya maana yake ni kuongezeka kwa
ukubwa wa kazi kwa upande wa wakaguzi, ogezeko ambalo litatupasa si
tu kufanya kazi kwa umakini mkubwa lakini pia kutekeleza majukumu
mengi na katika muda mfupi”.
Na
kwa sababu hiyo, akasema, kwa kutambua uzito na unyeti wa kazi kubwa
iliyombele, ndiyo maana baada ya kuteuliwa kwake yeye na maafisa wake
walianza jukumu la kujianda kwa kila hali ili waweze kulitekeleza
jukumu hilo kwa ukamilifu na weledi mkubwa.
Akatumia
fursa hiyo kuishukuru Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Afrika ya
Kusini kwa namna ambavyo imetoa ushiriano mkubwa na wa karibu sana,
kuanzia siku ile Ofisi ya NAOT ilipopitishwa kwa kauli moja na Baraza
Kuu la 66 la Umoja wa Mataifa kushika wadhifa huo.
Aidha
akasema ingawa Afrika ya Kusini imemaliza ujumbe wake, Tanzania
itaendelea kushirikiana nayo kwa karibu hasa kwa kuzingatia kwamba
kukabidhiwa kwa jukumu hilo hakuhitimishi mchakato mzima wa kuendelea
kubadilishana uzoefu na utaalamu.
Naye
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue akizungumza kwa niaba ya
serikali, pamoja na kuwashukuru wajumbe wa bodi ya UNBOA na
sekretarieti yake. Amesema Serikali inauchukulia ujumbe huo kwa uzito wa
aina yake.
“Nimefurahi
sana kuwapo hapa na kuiwakilisha serikali, ninapenda ninawakikishie
kwamba, serikali yangu inalipa jambo hilo uzito wa kipekee sana. Heshima
na mchango wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa unafamika na sasa
tunapoingia katika jukumu hili ni dhahiri kwamba tunataka kufanya kazi
nzuri hata katika maeneo mengine na uwezo huo tunao” akasisitiza.
Naye
Naibu Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu kutoka Afrika ya Kusini Bw. Thembekile
Makwetu akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, amemhakikisha Bw.
Utouh na ofisi yake ushirikiano wa karibu na usiotereka. Huku wajumbe
wengine wa Bodi nao wakielezea kutoa ushirikiano kwa Tanzani na
kuikaribisha kwa moyo mkunjufu.
Kwa
upande wake, Bi Susan Malcora akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa
Umoja wa Mataifa, yeye amesema anaikaribisha Tanzania katika ujumbe wa
bodi hiyo kwa mikono miwili na kusisitiza kwamba ujumbe wa Tanzania
katika Bodi hiyo utasaidi sana katika kusukuma mbele ajenda ya
uwajibikaji na udhibiti wa fedha na mali zinazomilikiwa na Umoja wa
Mataifa.
Akasema
Umoja wa Mataifa, unatambua umuhimu na mchango mkubwa wa Bodi hiyo na
kuongeza kwamba itafanya kazi kwa karibu wa wajumbe wa bodi ili
kuhakikisha kwamba mageuzi yanayoendelea hivi sasa ndani ya UM
yanafanyika kwa ukamilifu na kwamba watazingatia ushauri na maelekezo
watakayopewa na Bodi.
No comments:
Post a Comment