Wakati wabunge wakiendelea kujadili Bajeti ya Serikali ya mwaka 2012/13 iliyowasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa wiki iliyopita, siri nzito imefichuka, kwamba mishahara ya wabunge itaongezeka kuanzia Julai, mwaka huu.
Kwa mujibu wa kitabu cha bajeti namba 2 cha bajeti ya matumizi ya kawaida voti namba 2, kuanzia sasa bajeti ya Bunge imeongezeka kutoka Sh bilioni 77 hadi Sh bilioni 112 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 32.
Ongezeko la mishahara kwa wabunge, limekuja kutokana na pendekezo la Kamisheni ya Bunge la kuchukua posho ya vikao ambazo wabunge hulipwa na kuzihamishia katika mishahara yao ya kila mwezi.
Uchunguzi wa kina uliofanywa na MTANZANIA na kuthibitishwa na kitabu cha bajeti, kuanzia Julai mwaka huu mishahara hiyo itakapopanda, kila mbunge atakuwa anatia kibindoni Sh milioni 10 kwa mwezi.
Wakati wabunge wanapandisha mishahara yao, kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wafanyakazi wa Serikali, hasa walimu, madaktari, wauguzi, askari polisi na sekta nyinginezo.
ELIMU
Kwa mfano, sekta ya elimu imekuwa na matatizo makubwa ya wanafunzi kukosa vitabu, walimu kukosa nyumba na wanafunzi kulundikana kwenye vyumba vya madarasa kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa.
Jambo hilo limeonekana kuendelea kuwa sugu, licha ya juhudi kadhaa za Serikali zinazoendelea kuchukuliwa na mara kadhaa Serikali kusema haina fedha, ingawa mishahara ya wabunge inatarajiwa kupanda.
AFYA
Katika sekta ya afya, kumekuwa na tatizo kubwa la hospitali, vituo vya afya na zahanati kukosa dawa, huku wajawazito, watoto na wagonjwa mbalimbali wakiendelea kupata matatizo kwa kinachoelezwa kuwa serikali haina fedha za kununua dawa na vitanda vya kulalia wagonjwa.
Wakati Bunge likijiongezea bajeti yake kwa asilimia 32, wakati huo huo bajeti ya Serikali iliyowasilishwa bungeni ni asilimia 30 tu ndiyo imeelekezwa kwenye shughuli za maendeleo ambazo sehemu kubwa ya asilimia hiyo inatokana na mikopo.
Hali ikiwa hivyo, inaonyesha bajeti ya matumizi ni asilimia 70 ya bajeti nzima na sehemu kubwa ikiwa ni mikopo ya ndani na nje, jambo ambalo linaonyesha kuwa sehemu ya mikopo hiyo itaangukia katika kulipa mishahara ya wabunge.
Hali inaonyesha miradi mikubwa ya Serikali imesimama, huku makandarasi wakiendelea kuidai Serikali kutokana na kazi mbalimbali walizozifanya na Serikali kushindwa kuwalipa fedha kwa wakati.
Katika bajeti iliyopita, miradi mingi ilishindwa kutekelezwa na halmashauri nyingi zilikosa fedha za maendeleo, jambo ambalo liliathiri utendaji kazi wa madiwani.
Itakumbukwa kwenye bajeti hiyo, madiwani karibu nchi nzima walishindwa kushiriki kwenye vikao kwa sababu ya kukosekana fedha za kuwalipa posho.
SAKATA LA POSHO
Wakati mishahara hiyo ikipanda, mwaka jana Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliwaambia waandishi wa habari kuwa posho za wabunge zimepanda kutoka Sh 70,000 hadi Sh 200,000 kwa sababu hali ya maisha imepanda mkoani Dodoma ambako vikao vya Bunge hufanyika.
Lakini, kauli hiyo ilipingwa na Katibu wa Bunge, Dkt. Thomas Kashilillah, ambaye alisema posho hizo hazijapanda ingawa Spika alikuwa amesema zimeshapanda.
No comments:
Post a Comment